Mkurugenzi
wa Elimu kwa mlipa kodi toka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw.
Richard Kayombo akionesha kwa waandishi wa Habari leo Jijini Dar es
salaam moja ya CD zilizokamatwa wakati wa msako wa kubaini wale wote
wanaojihusisha na uuzaji na usambazaji wa kazi za wasanii bila kuwa na
stempu za kodi katika bidhaa za filamu na muziki. Kulia ni Katibu
Mtendaji wa Bodi ya Filamu Bi Joyce Fissoo na mwisho kulia ni Afisa
Habari wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Bi Mariam Mwayera.
Mkurugenzi
wa Elimu kwa mlipa kodi toka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw.
Richard Kayombo (katikati) akitoa wito leo Jijini Dar es salaam kwa
wasambazaji na wauzaji wa kazi za Filamu na muziki kuzingatia sheria na
Kanuni zinazosimamia sekta hiyo kwa kuwa Serikali itawachukulia hatua
kali wale wote watakaoenda kinyume cha sheria na taratibu zilizopo
ikiwemo kutozwa faini isiyopungua milioni tano au kifungo kisichopungua
miaka mitatu jela. Kulia ni Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Bi Joyce
Fissoo,Kushoto ni Afisa Utamaduni wa Bodi ya filamu Bw. Wilhadi Tairo.
Katibu
Mtendaji wa Bodi ya Filamu Bi Joyce Fissoo akifafanua kwa waandishi wa
habari leo jijini Dar es salaam kuhusu mikakati ya Bodi hiyo kuhakiksha
kuwa kazi za wasanii wa filamu zinaendana na maadili ya Taifa.kushoto ni
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania Bw. Richard Kayombo.
Baadhi
ya waandishi wa Habari wakifuatilia mkutano wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) na Bodi ya Filamu Tanzania ukilenga kueleza Mikakati ya
Serikali katika kulinda haki za wasanii wa filamu na Muziki zinalindwa.(
Picha na Frank Mvungi- Maelezo)
Na Fatma Salum (MAELEZO)
Serikali
kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeahidi kuendeleza msako wa
wafanyabiashara wote wanaouza kazi za filamu na muziki bila kubandikwa
stempu halali za kodi ili kuzilinda kazi hizo kwa ajili ya kuwanufaisha
wasanii na kuhakikisha Serikali inapata mapato yake.
Hayo
yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma kwa Mlipa Kodi kutoka TRA Richard
Kayombo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es
Salaam.
Kayombo
amesema TRA kwa kushirikiana na wadau wa tasnia ya muziki na filamu
imedhamiria kuhakikisha kuwa bidhaa za filamu na muziki zenye stempu za
kodi ndizo zinazoingizwa sokoni ili kulinda kazi za wasanii wa taifa
letu dhidi ya dhuluma zinazofanywa na baadhi ya wafanyabiashara.
“Msako
huu endelevu utahusisha kukamata bidhaa zote ambazo hazijabandikwa
stempu za kodi na kuwachukulia hatua wahusika kwa mujibu wa sheria.”
Alieleza Kayombo.
Aidha
Kayombo amefafanua kuwa kwa kipindi cha mwezi Februari na Machi 2016,
TRA kwa kushirikiana na Dalali wa Mahakama Yono Auction Mart &
Company Limited ilifanya msako jijini Dar es Salaam na kukamata jumla ya
CD na DVD zenye thamani zaidi ya shilingi Bilioni 1.3 ambazo
zilisambazwa bila kufuata sheria hivyo kukwepa kodi ya ushuru ipatayo
shilingi Milioni 31.9 na gharama za stempu zaidi ya shilingi Milioni
11.1.
TRA
inawatahadharisha wale wote wanaosambaza na kuuza kazi za filamu na
muziki ambazo hazijabandikwa stempu kuacha mara moja na kufuata
utaratibu wa kupata stempu hizo katika ofisi za TRA ili wawe na uhalali
wa kuuza bidhaa hizo kinyume chake hatua kali za kisheria zitachukuliwa
dhidi yao.
0 comments: