Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli
akikata utepe huku viongozi wengine wakiushikilia kuashiria uzinduzi
rasmi wa Daraja la Kigamboni katika wilaya mpya ya Kigamboni jijini Dar
es salaam leo Aprili 19, 2016.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli
akipata picha ya kumbukumbu viongozi wengine baada ya uzinduzi rasmi wa
Daraja la Kigamboni katika wilaya mpya ya Kigamboni jijini Dar es
salaam leo Aprili 19, 2016.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli
akiteta jambo na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Dkt Ramadhani Dau
wakati wa uzinduzi rasmi wa Daraja la Kigamboni katika wilaya mpya ya
Kigamboni jijini Dar es salaam leo Aprili 19, 2016.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 19 Aprili, 2016 amefungua
rasmi Daraja la Kigamboni linalounganisha usafiri wa barabara kati Kigamboni na
Kurasini Jiji la Dar es salaam na amependekeza Daraja hilo liitwe Daraja la Nyerere (Nyerere Bridge).
Sherehe za
ufunguzi wa daraja hilo kubwa na la kipekee kwa Afrika Mashariki na Kati zimefanyika
kando ya daraja hilo upande wa Kigamboni na kuhudhuriwa na viongozi na wageni
mbalimbali wakiwemo Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Balozi wa China nchini
Tanzania Dkt. Lu Youqing, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi
Mhandisi Edwin Ngonyani, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi,
Vijana, Ajira na Walemavu) Mheshimiwa Antony Mavunde,
Wabunge na Mameya wa Jiji na Dar es salaam.
Ujenzi wa daraja
hilo umehusisha nguzo mbili za pembezoni na mihimili miwili inayoshikilia nyaya
36, na daraja zima lina urefu wa meta 680, upana wa mita 32, njia sita za
magari, njia mbili za watembea kwa miguu na barabara unganishi zenye urefu wa
kilometa 2.5.
Daraja hilo
limejengwa kwa fedha za ndani na kugharimu jumla ya shilingi Bilioni 254.12
ambapo kati ya fedha hizo asilimia 60 zimetolewa na Shirika la Hifadhi ya Jamii
(NSSF), na asilimia 40 zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Kujengwa kwa
Daraja hili kutaondoa kero ya msongamano wa magari na usafiri kwa wakazi wa
Kigamboni na wakazi wa katikati ya Jiji la Dar es salaam ambao walilazimika
kutumia kivuko (Ferry) ili kukatiza eneo la mkondo wa bahari ya Hindi ama
kutumia barabara ya kuzunguka kupitia Kongowe lenye urefu wa kilometa 52.
Daraja hilo
limefanyiwa majaribio kwa kutumia Malori 44 yenye uzito wa tani 30 na
limethibitika kuwa na uwezo wa kubeba jumla ya tani 1,320 na hivyo linatarajiwa
kusaidia usafirishaji wa mizigo ya kutoka na kuingia katika bandari ya Dar es
salaam.
Akizungumza katika
sherehe hizo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
ameagiza vyombo husika vianze mchakato wa daraja hilo kupewa jina la "Daraja la Nyerere" (Nyerere Bridge) ikiwa ni kuuenzi
mchango mkubwa wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
aliyefanya kazi kubwa ya kuijenga Tanzania.
Aidha, Rais
Magufuli amewapongeza wadau wote waliohusika kufanikisha ujenzi wa Daraja hilo
likiwemo Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na
Uchukuzi na wakandalasi kutoka China, na ametaka watanzania wajivunie daraja
hilo kubwa na lililojenga heshima kubwa kwa nchi.
Pia Dkt. John
Pombe Magufuli ametoa wito kwa vyombo vya habari vya Tanzania kuitangaza vyema
Tanzania na kuwa na uzalendo wa kweli kwa nchi yao badala ya kubeza kazi nzuri
zinazofanywa ndani ya nchi kwa manufaa ya watanzania.
Katika
hatua nyingine Rais Magufuli amemsimamisha kazi
Mkurugenzi wa Jiji la Dar es salaam Bw. Wilson Kabwe na kuagiza vyombo
vinavyohusika kufanya uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili za kusaini
mikataba iliyosababisha serikali kupoteza mapato.
Dkt. Magufuli
ametangaza uamuzi huo wakati akitoa hotuba ya ufunguzi wa daraja la Kigamboni,
baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Bw. Paul Makonda kumueleza kuwa amebaini
upotevu wa shilingi Bilioni 3 uliotokana na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es salaam
Bw. Wilson Kabwe kusaini mikataba ya ukusanyaji mapato ya Kituo Kikuu cha
Mabasi Ubungo kwa kutumia sheria iliyopitwa na wakati, na pia ukusanyaji wa
tozo za uegeshaji wa magari ndani ya Jiji.
Gerson
Msigwa
Kaimu
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es
salaam
19 Aprili,
2016
0 comments: