Msimamizi
wa ujenzi wa Mradi wa bomba jipya la maji kutoka Ruvu Juu Mlandizi hadi
Dar es salaam lenye urefu wa km 40 ambalo liko katika hatua za mwisho
za ujenzi kutoka DAWASA Mhandisi Christian Gava akitoa ufafanuzi wa
masuala ya kiufundi kuhusu mradi huo. Kushoto ni Meneja Mawasiliano na
Uhusiano wa Jamii wa DAWASA Neli Msuya.
Wataalam
wa ujenzi kutoka DAWASA na kampuni ya Megha Engineering &
International Ltd inayojenga bomba jipya la maji kutoka Ruvu Juu
Mlandizi hadi Dar es salaam India wakiangalia moja ya matoleo 12
yanayopita chini ya barabara kuu ya Morogoro eneo la kimara.
Moja
ya daraja linapopitisha bomba hilo kutoka Ruvu Juu Mlandizi hadi Dar es
salaam lenye urefu wa km 40 linavyoonekana mara baada ya kukamilika eneo
la Kibamba.
Picha na Aron Msigwa- MAELEZO.
Na.Aron Msigwa - MAELEZO.
MAMLAKA
ya Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam ( DAWASA) imesema kuwa wakazi
zaidi wa jiji la Dar es salaam na Kibaha mkoani Pwani wanatarajia
kunufaika na huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama ifikapo Juni
mwaka huu kufuatia mradi wa ujenzi wa bomba jipya la maji kutoka Ruvu
Juu Mlandizi, Kibaha hadi jijini Dar es salaam kuwa katika hatua za
mwisho za ujenzi.
Meneja
Mawasiliano na Uhusiano wa Jamii wa DAWASA Neli Msuya ameyasema hayo
leo jijini Dar es salaam mara baada ya kutembelea eneo Kimara na Kibamba
ambako mafundi wa Kampuni inayojenga mradi huo ya Megha Engineering
& International Ltd kutoka India wanaendelea na kazi ya ujenzi wa
madaraja na matoleo ambayo bomba hilo linapitia katika barabara ya
Morogoro.
Amesema
hadi kukamilika kwake mradi huo utagharimu kiasi cha dola za Kimarekani
milioni 59.3 na utawezesha kiasi cha Lita milioni 196 za maji
kusafirishwa kwa siku ambazo zitaongezwa kwenye lita milioni 270
zinazozalishwa kwa siku na Mtambo wa Maji wa Ruvu Chini ulioko Bagamoyo
mkoani Pwani.
Ameeleza
kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaondoa kabisa tatizo la uhaba wa maji
katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam ambayo yameunganishwa
na mtandao wa mabomba ya DAWASCO ambayo yalikua hayapati maji kwa muda
mrefu au kupata kwa mgawo kufikia mwezi Juni, 2016.
Bi.
Neli amesema kuwa ili kuhakikisha mradi huo unakamilika katika kipindi
kilichopangwa na kuanza kuwanufaisha wananchi, ujenzi wake unakwenda
sambamba na umaliziaji wa tenki jipya la kuhifadhia maji lililoko eneo
la Kibamba lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni 10 ambalo ujenzi
wake umekamilika kwa asilimia 98.
Aidha,
amesema kuwa kazi ya ukarabati wa matenki ya zamani yaliyoko eneo la
Kimara jijini Dar es salaam inaendelea sambamba na ubadilishaji wa
mifumo ya mabomba ya zamani ambayo sasa ni chakavu ili iweze kuhimili
wingi wa maji uliopo.
"
DAWASA tumeshaingia mkataba na Mkandarasi kwa ajili kulaza upya mabomba
ya maji kwa wananchi wasiounganishwa na maji ili waweze kuingia kwenye
mtandao wa mabomba yetu, kazi hii inaendelea katika maeneo mbalimbali
ikiwemo Kimara, Mlandizi,Kibaha, Kwembe, Segerea, Changanyikeni, Mbezi
na Makuburi" Amesema.
Bi.
Neli ameongeza kuwa baadhi ya maeneo yataanza kupata mabadiliko ya
huduma ya maji kuanzia mwezi Mei kufuatia maji yatakayosukumwa kutoka
Ruvu, Mlandizi kuanza kutoka katika kituo cha kwanza kwenye tenki la
maji la Kibamba.
“Tunatarajia
wananchi waliounganishwa na mtandao wataanza kuona mabadiliko kuanzia
mwezi Mei, japo sasa kuna maeneo yana mgawo wa Dawasco,lakini baada ya
maji haya kufika na kuanza kutoka kwenye kituo cha tenki la Kibamba
wananchi watakua na maji ya kutosha" Amesisitiza.
Kwa
upande wake Msimamizi wa ujenzi wa Mradi huo kutoka DAWASA Mhandisi
Christian Gava akitoa ufafanuzi wa masuala ya kiufundi kuhusu mradi huo
amesema kuwa ili kukamilisha ujenzi wa mradi huo imewalazimu kujenga
maungio 15 ambayo bomba hilo linavuka mito na matoleo 12 yanayopita
chini ya barabara kuu ya Morogoro.
Amesema
kazi ya wekaji wa miundombinu ya kulifanya bomba lipite juu ya mto
kupitia madaraja yaliyojengwa imefanyika kwa umakini mkubwa ili kuepuka
kuathiri uasili wa mito husika.
Aidha,
amesema kuwa ili kulinda bomba hilo na athari za mafuriko katika mito
hiyo ulifanyika utafiti maalum ukihusisha upimaji wa kimaabara wa udongo
ili kubaini namna udongo huo unavyoweza kubeba nguzo kubwa zilizoshika
bomba hilo.
Mhandisi
Gava ameongeza kuwa ujenzi wa tenki la maji lenye uwezo wa kuhifadhi
lita milioni 10 umekamilikia kwa 98 na kubainisha kuwa kilichobakia ni
umaliziaji wa kazi ndogondogo.
“Ujenzi
wa Tenki umekamilika, hatua inayofuata ni kukamilisha kazi ndogondogo
kisha kulijaza maji kama sehemu ya uangalizi na taratibu za kiufundi,
Tunatarajia wiki ijayo tutajaza maji" Amesisitiza Mhandisi Gava.
0 comments: