Kaimu
Meneja wa Idara ya Takwimu za Ajira na Bei wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu
(NBS) Bi. Ruth Minja akitoa ufafanuzi kwa wahariri wa vyombo vya Habari
kuhusu matokeo ya Utafiti wa Watu wenye uwezo wa kufanya Kazi leo jijini
Dar es salaam. Matokeo hayo yataiwezesha Serikali kuangalia upya tija
ya utendaji kazi katika shughuli zinazofanywa na makundi mbalimbali ili
kubaini mchango wake katika kukuza Pato la Taifa.Picha na Aron Msigwa
–MAELEZO.
Baadhi ya
Wahariri na Waandishi wa Habari waliohudhuria ufafanuzi kwa wahariri wa
vyombo vya Habari kuhusu matokeo ya Utafiti wa Watu wenye uwezo wa
kufanya 2014 Kazi leo jijini Dar es salaam.
Baadhi ya
wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari na waandishi wa habari
wakisikiliza maelezo wakati wa uwasilishaji wa matokeo hayo ya utafiti
wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi mwaka 2014.
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Dar es salaam.
Ofisi ya
Taifa ya Takwimu (NBS) imesema kuwa takwimu za matokeo ya utafiti wa
Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa Mwaka 2014 zitatumika kufanya
maboresho ya Mipango na Sera mbalimbali za kukuza ajira na kupunguza
umasikini nchini.
Matokeo
ya utafiti huo yameonesha kuwa asilimia 70.9 ya muda wa watu wenye umri
wa miaka 15 au zaidi kwa siku hutumika kwenye shughuli zisizo za
uzalishaji ikilinganishwa na asilimia 18.5 inayotumika kwenye shughuli
za kiuchumi.
Akizungumza
na wahariri wa vyombo vya habari leo jijini Dar es salaam Kaimu Meneja
wa Idara ya Takwimu za Ajira na Bei wa Ofisi hiyo Bi. Ruth Minja amesema
kuwa matokeo hayo yataiwezesha Serikali kuangalia upya tija ya utendaji
kazi katika shughuli zinazofanywa na makundi mbalimbali ili kubaini
mchango wake katika kukuza Pato la Taifa.
Amesema
kwa mujibu wa utafiti huo Tanzania ina nguvu kazi ya Taifa ya watu
milioni 22.3 wanaume wakiwa milioni 11 na wanawake wakiwa milioni 11.2
huku idadi ya watanzania walio nje ya nguvu kazi ya Taifa wakifikia
milioni 3.4.
Amefafanua
kuwa idadi ya watanzania walio kwenye ajira ni milioni 20
ikilinganishwa na watu milioni 2.2 ambao hawako kwenye ajira huku
akibainisha kwamba kiwango cha nguvu kazi iliyo katika uzalishaji wa
bidhaa na huduma za kiuchumi na nguvu kazi iliyo tayari kujihusisha na
uzalishaji mali kimepungua kutoka asilimia 89.6 mwaka 2006 hadi asilimia
86.7 ya mwaka 2014.
Kwa
mujibu wa utafiti amesema kiwango cha watu wenye umri wa kufanya kazi
walio na ajira kwa upande wa wanaume kwa mwaka 2006 kilifikia asilimia
80.8 ikilinganishwa na asilimia 82.1 za mwaka 2014 huku kiwango hicho
hicho kwa upande wa wanawake kwa mwaka 2014 kikifikia 73.8 kutoka 77.6
za mwaka 2006.
“ Kiwango
cha watu wenye umri wa kufanya kazi walio na ajira kwa ujumla
kimepungua, hii inaonesha kuwa, kiwango cha uchumi kuzalisha ajira
kimepungua kidogo kutoka asilimia 79.2 mwaka 2006 hadi asilimia 77.8
mwaka 2014” Amesema.
Kuhusu
masaa ya kufanya kwa watu wenye umri wa miaka 15 na kuendelea Bi. Ruth
Minja amesema kuwa kati ya mwaka 2006 hadi 2014 kumekuwa na ongezeko la
masaa ambayo watu hufanya kazi kwa makundi yote ya ajira akifafanua kuwa
watu wanaofanya kazi kwa malipo na waliojiajiri wamekuwa wakifanya kazi
zaidi ya saa 50 kwa wiki kuliko hali nyingine za ajira.
“ Napenda
kuwaeleza kuwa takwimu hizi zitasaidia kuboresha sera ya ajira na
programu nyingine ili kuwe na uwiano kati ya saa za watu wanaofanya
kazi, uzalishaji na malipo wanayopewa” Amesisitiza.
Aidha,
amefafanua kuwa kwa upande wa ukosefu wa ajira kwa muda mrefu kwa watu
wenye umri wa miaka 15 au zaidi kote nchini wananwake wana kiwango
kikubwa cha ukosefu wa ajira kuliko wanaume kwa miaka yote ya utafiti
uliofanywa na Ofisi hiyo toka mwaka 2006 hadi 2014.
Amesisitiza
kuwa ipo haja kwa Serikali na wadau mbalimbali kushughulikia kiwango
cha watu wasio na kazi na wale ambao hawako tayari kufanya kazi yoyote
ya kiuchumi kutokana na ongezeko lake kuwa kubwa kutokana na athari yake
kwa uchumi wa taifa.
“
Kiashiria hiki katika utafiti tulioufanya kinabainisha kuwa kiwango cha
watu ambao hawakuwa na kazi wala hawakuwa tayari kufanya kazi yoyote ya
kiuchumi kimeongezeka kutoka ailimia 10.4 za mwaka 2006 hadi 17.2 za
mwaka 2014 “ Amesisitiza.
Ameeleza
kuwa kufuatia kiashiria hicho wanawake wana kiwango kikubwa zaidi kuliko
wanaume kwa kuwa wao hujishughulisha na shughuli za nyumbani ambazo sio
za kiuchumi zikiwemo za kufua nguo, kupika na malezi ya watoto.
0 comments: