Na Mwandishi Wetu
BIASHARA
ya kusafirisha mazao ni miongoni mwa biashara zenye ushindani mkubwa
kutokana na kutawaliwa na matajiri wenye asili ya Kiasia.
Kutokana
na sababu hiyo imewafanya waafrika wengi kuwa na uthubutu katika
biashara kwa kuhofia huenda wasifanikiwe na kujitanua kibiashara.
Mbali
na ugumu huo lakini pia waafrika wengi hasa watanzania wamejikuta
wakiishia kuwa wafanyabiashara ya kawaida na kupoteza fursa za
kimataifa .
Kupoteza
fursa muhimu za kimataifa kumefanya wakose fursa ambazo zingeweza
kuwafanya wawe na mawazo mengine ya kuchangamkia fursa za kibiashara na
kufikiri nje ya boksi.
Makala
haya ndani ya mtandao huu yanaangazia mahojiano na mfanyabiashara wa
kwanza wa kitanzania kufanya biashara ya kusafirisha Korosho kwenda
nchini Vietnam aitwaye Abbas Maziku ambapo alielezea alipoanzia,
vikwazo, mafanikio na matarajio yake kibiashara.
Alipoanzia
Maziku
anasema alianza biashara ya kusafirisha mazao mnamo mwaka 2013 baada ya
kuvutiwa na mjomba yake ambaye alikuwa na mashamba yaliyokuwa na
mazao mbalimbali.
Miongoni
mwa mazao ambayo Maziku alianza nayo na anaendelea nayo ni pamoja na
Korosho, Ufuta, Mbaazi, Choroko, Mtama, Alizeti, Mashudu yapamba na
pamoja na Pilipili Manga.
Anayapata wapi mazao?
Anasema
mazao huyakusanya kutoka kwa wafanyabaishara wadogo wadogo ambao
hukusanya mazao kwa wakulima pamoja na minada inayofanywa na vyama vya
ushirika katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Dodoma, Singida, Shinyanga na
Tanga ambayo hufanyika mara moja kwa kila wiki.
Anayasafirisha kwa njia gani?
Akizungumzia
jinsi anavyosafirisha mazao hayo, Maziku anasema hutumia usafiri wa
barabara kuyatoa mikoani hadi kuyafikisha kwenye maghala ambayo hutumia
kuyahifadhi kabla ya kufungasha.
“Wakati
wa kuyafungasha unapofika huwa nayafungasha kwa kutumia vibarua na
katika vifungashio vyangu huwa na nembo inayoonyesha jina la kampuni
yangu na baada ya hapo sampuli hupelekwa katika maabara za kupima
kupima ubora wa mazao kimataifa iitwayo SGS na ndipo hufuatiwa na hatua
ya mwisho ya usafirishaji ambayo huwa natumia Meli za mashirika
mbalimbali ikiwemo IPTL, MAERSK na nyinginezo kwa ajili ya kwenda
nchini Vietnam”, anasema Maziku.
Anabainisha
baada ya hatua zote hizo hufuata taratibu zinazotakiwa ikiwemo watu wa
Mamlaka ya mapato T.R.A, wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo na Ufugaji,
Wanasheria pamoja na maofisa wa usalama wa Taifa ambao uhakikisha hatua
zote halali zimefutwa.
Maziku
anaweka bayana kwamba kwa biashara za kimataifa taasisi kama
Shirika la viwango TBS na mamlaka ya Chakula na Dawa huwa hawahusiki
bali wahusika wakuu ni SGS.
Anajiendeshaje Kibiashara?
Maziku
anajinasibu kuwa biashara ya mazao kupeleka nje ya nchi ni biashara
yenye ushindani mkubwa hivyo anakumbuka alianza na mtaji wa sh 2,000,000
na sasa anazungumzia mtaji wa sh mil 200.
“Si
rahisi kufika nilipofikia kwa sababu biashara hii ina ushindani
mkubwa, ninashindana na matajiri wakubwa wenye uwezo wa kujipangia bei
za mazao hivyo ingawa nimepiga hatua lakini bado ninahitaji kupanua
biashara yangu zaidi na zaidi”, anasisitiza kwa hisia kali.
Anaeleza
kuwa mwaka 2013 alipata hasara ya mamilioni ya pesa baada ya ubora wa
mazao kupimwa na kuonekana upo kwenye kiwango cha 48 badala ya 51
inayotakiwa hivyo ilimpa wakati mgumu ambao aliyumba kibiashara
kutokana na mtaji wake kukata hivyo ili mlazimu kuingia benki na
kukopa pesa ambazo hadi sasa bado analipa deni hilo.
“Nilipata
hasara kubwa sana ambayo hadi leo hii bado ninalipa hilo deni
nililokopa benki ingawa pia fedha kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vya
mapato ya biashara zingine ninazozifanya zinaendelea kuifanya biashara
hii ya mazao kwenda nje ya nchi iendelee kuwepo” anasema Mfanyabiashara
huyo wa kimataifa.
Vikwazo vya kibiashara
Maziku
anakwenda mbali zaidi na kueleza kuwa katika jambo lolote lenye
mafanikio, hasa biashara vikwazo huwa havikosekani lakini kubwa katika
biashara za kimataifa ni mitaji.
Hapa
analia na ukiritimba unaofanywa na benki mbalimbali ambazo hutaka
dhamana kubwa kuliko uwezo wa mfanyabiasahara hivyo hilo ni tatizo
linalokwaza ukuaji wa biashara.
Ukiachilia
mbali suala la benki, Maziku anasema kikwazo kingine ni Ukiritimba
uliopo kwenye vyama vya ushirika katika suala zima la upangaji wa bei
ambao wakati mwingine unakinzana na bei ya katika soko la dunia hivyo
inakuwa ni vigumu kwa wafanyabiashara kufikia malengo kutokana na
kuepuka kupata hasara.
Aidha
anataja vikwazo vingine ni wizi wa fedha unaofanywa baada ya kuwaamini
watu wa kuwanunulia mazao na badala yake hutoroka na fedha hivyo
kufanya suala la uaminifu kuwa mdogo mbali ya vikwazo vya ubora wa
mazao wakati mwingine hayawi katika viwango na ubora unaotakiwa.
Mfanyabiashara wa Kimataifa Abbas Maziku akiwa ofisini kwake maeneo ya Posta mpya jijini Dar es salaam.
Mafanikio
Akizungumzia
mafanikio Maziku anabainisha kuwa, tangu alipoanza biashara ameweza
kuwa na kampuni mbili zijulikanazo kama GEFU Agromart Company Limited
na Lyone Investment Company Limited ambazo kwa pamoja ameajiri
wafanyakazi watano wakiwemo Ofisa rasilimali watu, Mhasibu, Katibu
Muhtasi, Mwanasheria na Meneja Mwendeshaji wa shughuli za kampuni.
Anaeleza
kuwa kwa biashara anayoifanya ameweza kujenga nyumba yake mwenyewe,
kuwa na usafiri wake pamoja na kupata fursa za kusafiri kwenda nchi
mbalimbali kuhudhuria makongamano na maonyesho ya biashara ya mazao
jambo ambalo limemkutanisha na watu mbalimbali na kupanua wigo wa
biashara yake kimataifa.
Matarajio yake
Maziku
anaeleza kuwa anataraji kufungua kampuni ya ujenzi ili mtaji wake
uzunguke pamoja na kutoa ajira kwa vijana mbalimbali wa Kitanzania .
Mbali
ya hilo pia matarajio yake ya baadaye ni kuanzisha kiwanda cha
uzalishaji wa bidhaa ndogo ndogo za majumbani kama vile juisi, mafuta
ya alizeti , mifuko ya rambo pamoja na maji ya kunywa kwa ushirikiano
baina yake na wawekezaji kutoka nje kwa lengo moja tu la kukuza uchumi
wa Tanzania .
Anajihusishaje na masuala ya kijamii?
Maziku
anabainisha kuwa anajihusisha kikamilifu na masuala ya kijamii hasa
kusaidia wasiojiweza ikiwemo yatima lakini mambo hayo huyafanya nyuma
ya pazia pasipo kujitangaza.
“Kidogo nilicho nacho huwa nakitoa kwa wenye mahitaji maalum lakini huwa sijitangazi “anasisitiza Mjasiriamali huyo
Abbas
Maziku akiwa katika moja ya shughuli zake za kusafirisha mazao kuelekea
mataifa mbalimbali katika Bandari ya Mtwara kama makontena
yaliyohifadhiwa mazao hayo yanavyoonekana nyuma yake.
Maziku ni nani?
Maziku ni kijana wa Kitanzania mwenye asili ya kabila la Wasukuma ambaye alizaliwa mwaka 1990. Ni kijana wa mwenye umri mdogo ikilinganishwa na mafanikio yake kibiashara. Kitaaluma
Maziku ni Mtaalamu wa masuala ya benki na fedha ambayo aliipata
katika Chuo kikuu cha Zanzibar miaka kadhaa iliyopita na pia aliwahi
kuwa mfanyakazi wa benki ya Exim kama ofisa wa kawaida wa Benki ambayo
alidumu nayo kwa muda mfupi sana na kugeukia katika biashara ya mazao.
Kimsingi
Maziku ni mtoto wa tatu na wa mwisho kutoka katika wazazi wake na ndoto
yake ni kuwa mfanyabiashara mwenye umri mdogo mwenye mafanikio makubwa
kama Mohammed Dewji ‘MO’ ambapo anatamani kufikia mafanikio kama hayo,
kwani anaamini kujituma na kuweka malengo katika biashara ni nguzo ya
kufiki malengo.
Ushauri
Maziku
anawashauri vijana wenzake kuwa na uthubutu alionao yeye, aliiona fursa
akaichangamkia na hadi kufikia alipo ingawa bado mapambano
yanaendelea.
“Vijana
tusibweteke,vikwazo ni vingi, hatupaswi kukata tamaa, hata
waliofanikiwa kama akina MO hawakuanzia juu, walipambana na uzuri ni
kwamba MO si mchoyo, ni mtu anayejitoa, mwenye msaada katika mambo
mbalimbali ya ushauri wa kibiashara jambo ambalo linanifanya niwe ni mtu
ninayemuheshimu na amechangia katika mafanikio yangu ya kibiashara
hivyo sitaacha kumshukuru,na pia ningependa kumshukuru Rais wangu Jakaya
Kikwete kwa kuwa miongoni mwa watu waliochangaia mafanikio yangu ya
kibiashara” anahitimisha Maziku .
Magunia
ya Korosho yakisubiri kupakiwa kwenye Makontena tayari kwa
kusafirishwa kwenda nchini Vietnam ambapo Mfanyabiashara Abbas Maziku
hufanya nao biashara kwa mkataba maalum.
0 comments: