Kwa akali watu sitini wameuawa baada ya kundi la watu linalosadikiwa kuwa la Boko Haram kushambulia vijiji viwili vilivyoko katika jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria. Baba Shehu Gulumba,
Kiongozi wa kieneo katika mji wa Bama amesema kuwa, shambulio hilo limepelekea idadi ya raia wengine kadhaa kujeruhiwa. Kiongozi huyo ameeleza kuwa, mara baada ya wanamgambo hao wa kundi la Boko Haram kufanya shambulio hilo la kinyama, walichoma moto nyumba za wanavijiji.
Baba Shehu Gulumba amesema kuwa, jambo la kushangaza ni kwamba wanamgambo hao wa Boko Haram walishambulia maeneo hayo kwa kutumia magari ya serikali. Shambulio hilo limefanyika katika hali ambayo, siku ya Jumapili wanamgambo wanaobeba silaha waliua watu wasiopungua 19 katika miji miwili nchini humo. Inafaa kuashiria hapa kuwa, mwezi Mei mwaka jana, Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria alitangaza hali ya hatari katika majimbo matatu ya Borno, Yobe na Adamawa.
0 comments: