Thursday, March 20, 2014

at 12:14:00 AM  |  No comments

Rais Joseph Kabila
 Rais Joseph Kabila 
 
Jitihada za chama tawala cha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) za kutaka kuifanyia marekebisho katiba zimezusha mjadala mkubwa nchini humo. Mrengo wa upinzani sambamba na kupinga uamuzi huo, umemtuhumu Rais Joseph Kabila kuwa amepuuza demokrasia na anapenda madaraka. Wafuasi wa kiongozi huyo wa Kongo wanakusudia kuifanyia marekebisho katiba ili kumuandalia njia ya kugombea tena katika uchaguzi ujao wa rais. Uchaguzi wa rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo utafanyika mwaka 2016. Wapinzani wanasema jaribio hilo la kutaka kubadili katiba ni sawa na 'mlipuko wa bomu'.


Chama tawala cha Kongo kinataka kuiga katiba ya Afrika Kusini kwa kufanyia marekebisho kipengee nambari 220 cha katiba, ili kumuwezesha rais wa nchi kuongoza kwa vipindi vitatu. Wawakilishi wa kambi ya upinzani katika Bunge la Kongo wanasema kuwa, uamuzi huo unakinzana na katiba yenyewe kwani kwa mujibu wa katiba ya DRC rais anaweza kuongoza nchi kwa vipindi visivyozidi viwili vya miaka mitano mitano. Wapinzani wamepania kuanza kuwahamasisha wananachi ili kuzuia marekebisho hayo.
 Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa, hitilafu kuhusu kufanyiwa mabadiliko katiba katika hali ya hivi sasa zitazidisha malalamiko ya wananchi. Katika upande mwingine, hitilafu zilizojitokeza kati ya wafuasi wa chama tawala juu ya marekebisho ya kipengee nambari 220 cha katiba ya Kongo ni kadhia nyingine inayozidisha wasiwasi kuhusu mustakbali wa nchi hiyo.

Wasiwasi unaripotiwa katika siasa za Kongo katika hali ambayo maafisa wa Umoja wa Mataifa hivi karibuni walitangaza kuwa vikosi vya jeshi la serikali vimedhibiti sehemu kubwa ya ardhi ya nchi hiyo kutoka kwa makundi ya waasi. Inasemekana kuwa, serikali ya Kinshasa imekomboa asilimia 80 ya ardhi iliyokuwa ikidhibitiwa na waasi waliolazimika kurejea nyuma.

        Jeshi la taifa la Kongo tangu Januari 16 mwaka huu lilianza operesheni ya kijeshi kwa lengo la kuhitimisha harakati za waasi, wakiwemo waasi wa Uganda wa ADF Nalu katika nchi hiyo. Harakati ya Mach 23 pia ni miongoni mwa makundi makubwa ya waasi wa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambalo lililazimika kuhitimisha rasmi shughuli zake baada ya kushindwa mtawalia. Japokuwa bado kuna makundi mengine ya waasi yanayoendesha harakati mashariki mwa Kongo, lakini serikali ya Kinshasa imepata mafanikio makubwa. Weledi wa mambo wanasema kuwa, kwa kuzingatia hali hiyo hitilafu zilizozuka katika uga wa kisiasa na kudhoofika serikali kuu huenda kukazidisha harakati za waasi na kuzusha tena machafuko mashariki mwa Kongo.

Vilevile mgogoro wa ndani wa kisiasa utaandaa uwanja kwa nchi jirani na madola ya kigeni kuingilia zaidi masuala ya ndani ya Kongo. Kwa utaratibu huo, viongozi wa nchi za Magharibi wanaohesabiwa kuwa ndio chanzo cha migogoro na mapigano katika bara la Afrika hasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, watapata kisingizio kizuri cha kuhalalisha kuwepo katika eneo hilo ili kupora maliasili za nchi hiyo.

Share
Posted by Unknown
About the Author

Write admin description here..

0 comments:

Text Widget

Blogger templates. Proudly Powered by Blogger.