Friday, March 21, 2014

Mauaji Darfur vita vikitokota

at 10:52:00 AM  |  No comments

Mauaji Darfur vita vikitokota

 21 Machi, 2014 - Saa 15:04 GMT
Askari wa Sudan
Askari wa kikosi cha Sudan katika jimbo la Darfur
Shirika la haki za binadamu Human Rights Watch linasema makumi kadhaa ya watu waliuawa katika ghasia zinazoendelea katika jimbo la Darfur nchini Sudan.
Shirika hilo linasema viongozi wa kijamii katika vijiji viwili wametoa orodha ya majina ya raia takriban arobaini waliouawa katika wiki chache zilizopita kwenye makabiliano baina ya vikosi vinavyounga mkono serikali na vile vya waasi.
Human Rights Watch linasema wanavijiji wengine makumi kadhaa walishambuliwa, baadhi yao wakipigwa na makombora ya ndege za kijeshi. Shirika la msalaba mwekundu limesema mmoja wa wafanyakazi wake aliuawa jana.
Umoja wa Mataifa unasema mwaka huu pekee zaidi ya watu laki mbili wameyakimbia makazi yao jimboni Darfur.
Makao makuu EAC kwafukuta
Mwandishi Wetu
Toleo la 338
12 Feb 2014
Katibu Mkuu EAC, Dk. Richard Sezibera
MSUGUANO wa kidiplomasia unaoendelea kati ya Tanzania na Rwanda, umezidi kupanuka hadi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Raia Mwema likifahamishwa kwamba, baadhi ya wafanyakazi wameanza kumtuhumu Katibu Mkuu Dk. Richard Sezibera kuwaburuza kwa kuegemea zaidi matakwa ya nchi yake, Rwanda.
Gazeti hili limenasa baadhi ya mawasiliano ya barua pepe kati ya wafanyakazi wa Jumuiya hiyo wakishinikiza kuchukuliwa kwa hatua zaidi huku Dk. Sezibera akizuia kuendelea kwa mjadala huo na wakati huo huo Msemaji wa EAC, Owoora Richard Otieno, akiita madai hayo ni majungu.
Hali hiyo inajitokeza ikiwa ni zaidi ya miezi sita sasa Tanzania na Rwanda zimekuwa katika msuguano wa kidiplomasia, kutokana na ushauri uliotolewa na Rais Jakaya Kikwete wa kuitaka nchi hiyo jirani kukaa meza ya majadiliano na waasi wa kikundi cha FDRL.
Rais Kikwete alitoa ushauri mjini Addis Ababa wakati wa mkutano wa viongozi wa Umoja wa Afrika (AU) lakini alijikuta akishambuliwa na Rais Paul Kagame wa Rwanda, pamoja na vyombo vya habari vya nchi hiyo.
Taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki zinadai kuwa, wafanyakazi wa nchi hizo mbili wamekuwa “wakisigana” huku kila upande ukichukua msimamo wa nchi zao.
Mgogoro baina ya wafanyakazi hao pia unadaiwa kumhusisha Katibu Mkuu wa Sekretarieti hiyo ya EAC, Dk. Richard Sezibera, ambaye pia ni raia wa Rwanda, akilalamikiwa na baadhi ya watumishi kuwa  amekuwa akitekeleza majukumu yake kwa kuegemea upande moja.
Taarifa zaidi zinadai kuwa Dk.Sezibera ameshindwa kutoa mwongozo kwa viongozi  wa juu wa nchi wanachama hasa katika  utekelezaji wa miradi ya miundombinu, ikiwamo ujenzi wa reli, kati ya nchi za Kenya, Uganda na Rwanda, ambayo Tanzania na Burundi zimetengwa.
Ujenzi wa mradi huo ulizinduliwa mwaka jana mjini Mombasa na viongozi wa nchi zote tatu huku Tanzania na Burundi zikitengwa bila ya kuarifiwa hatua iliyosababisha nchi hizo mbili kuomba maelezo kutoka sekretarieti ya jumuiya.
“Utekelezaji wa mradi huo ulifikiwa na viongozi wakuu wa nchi tatu kwa matakwa ya kisiasa kinyume kabisa cha mkataba unaounda jumuiya hiyo”
“Matarajio ya wengi ni kwamba katibu mkuu na wasaidizi wake wangeingilia kidiplomasia kuwashauri viongozi wakuu wa Rwanda, Uganda na Kenya,” kilieleza chanzo chetu kutoka ndani ya EAC.
Mtoa habari wetu huyo alifafanua kuwa sura 7(3)ya mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo inaruhusu nchi wanachama kufanya miradi ambayo haiko kwenye mipango ya pamoja lakini ina manufaa katika  mtengemano wa jumuiya hiyo.
Inafahamika kuwa viongozi wa Kenya, Rwanda na Uganda wanatekeleza miradi ambayo imo katika mipango ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, tena bila kuomba idhini kwa nchi za Tanzania na Burundi ambazo ni wanachama wa jumuiya hiyo.
Kwa mfano suala la ujenzi wa miundombinu kama reli na barabara, upanuzi wa bandari, mkataba wa kukusanya ushuru kwa pamoja (single customs territory), hati moja ya kuingia na kukaa katika nchi wanachama kwa muda maalumu (single visa) na hata shirikisho la kisiasa.
“Mambo yote haya yamo katika mipango waliyokubaliana nchi wanachama na kila nchi ilikuwa inayafanyia kazi, lakini ghafla Rwanda, Kenya na Uganda zikaitana na kukubaliana kuyafanyia kazi kwa haraka. Hili jambo linatishia uwepo wa jumuiya,” alieleza.
Kimsingi, katibu mkuu wa EAC alipaswa kuzionya nchi hizo tatu kwa kuvunja mkataba wa jumuiya, lakini inadaiwa hakufanya hivyo kwa sababu nchi yake ya Rwanda ni mnufaika na miradi hiyo.
Mtendaji huyo mkuu wa jumuiya analaumiwa  kufanya kazi kwa kuegemea upande mmoja katika jambo hilo, kinyume cha mkataba wa Jumuiya unaowataka katibu mkuu wa EAC na wafanyakazi wa chini yake kutopendelea upande wowote.
Hali hiyo iliibua majibizano makali miongoni mwa watumishi wa jumuiya hiyo kupitia mtandao wa mawasiliano wa barua pepe, ukimhusisha pia katibu mkuu.
Mawasiliano hayo ambayo Raia Mwema imeyaona yanaonesha kuwa wengi wa watumishi walitaka sekretariati ya jumuiya ifanye jitihada za dhati kuokoa jumuiya isivunjike lakini Dk. Sezibera alitoa amri mjadala huo usitishwe.
Mmoja wa watumishi wa ngazi za juu katika Jumuiya, alionya kwenye barua pepe kwa kuandika; “Hatuwezi kukaa na kuangalia mambo yanavyokwenda na kuhatarisha uhai wa Jumuiya kama kweli sisi tunawaza kwa niaba ya Jumuiya….hivi ndivyo Jumuiya ya awali ilivyovunjika, kwa nini turuhusu ivunjike tena wakati wananchi wamekwishaona manufaa ya Jumuiya hii?” alihoji.
Mfanyakazi mwingine ambaye ni raia wa Kenya aliandika: “Labda Katibu Mkuu (SG) anapaswa kuwaita wafanyakazi wote walioko nje ya kituo ili kuunganisha vichwa na kutoa mwelekeo”.
“Hatuwezi kamwe kufukia vichwa vyetu kwenye mchanga kama vile hakuna kilichotokea. Tunawahitaji makatibu wakuu waliopita, marais wastaafu, Mwinyi, Mkapa na Moi na jopo la watu wanaoheshimika katika jamii kuweka mkakati wa kuiokoa jumuiya.”
Naye mfanyakazi mwingine mbali na hayo aliandika; “Itakuwa ni historia mbaya kuiacha Jumuiya ivunjike mikononi mwetu, bila kufanya jitihada zozote za kumaliza tofauti zilizoibuka. Hakika historia itatuhukumu vibaya”.
Hata hivyo akijibu hoja za wafanyakazi hao Katibu Mkuu wa Jumuiya katika barua pepe yake aliandika: “Masuala ya kidiplomasia huwa hayashughulikiwi kwenye mijadala  isiyokuwa na maana ya kwenye barua pepe”.
Akaendelea; “Sasa ninaagiza wafanyakazi wote wasijadili, wasitoe maoni kati ya nchi wanachama kwa namna yoyote ile, acheni idara zinazohusika na haya masuala kuyashulikia kwa utulivu.”
Aidha Dk. Sezibera pia analalamikiwa  kwa kuwabagua wafanyakazi wanaotoka Tanzania ambapo hivi karibu anadaiwa kumwondoa moja wa wasaidizi wake wa karibu ambaye ni Mtanzania akimtuhumu kuwa anampeleleza.
Mtumishi huyo (jina linahifadhiwa)  tayari ameondolewa kumsadia Katibu Mkuu huyo na inaelezwa kuwa amepangiwa kazi nyingine baada ya juhudi za kumfukuza  kazi  moja kwa moja kukwama.
Kwa upande wake msemaji wa EAC, Owoora Richard Otieno alipuuza madai hayo  na kuyaita “majungu” yasiyo na tija kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Hii ni taasisi inayoendeshwa kitaalamu, na watumishi wote ni wataalamu wa kiwango cha juu, na Katibu Mkuu hana mamlaka ya moja kwa moja kumfukuza mtumishi yoyote,” alisema.
Kuhusu suala la Tanzania na Burundi kutengwa katika miradi kadhaa msemaji huyo alifafanua kuwa hata Tanzania ina miradi ya pamoja na baadhi ya nchi wanachama.
Akitoa mfano Owoora alieleza kuwa Tanzania ina mradi wa pamoja wa kujenga kituo cha kuzalisha umeme katika mto Rusumo na ujenzi wa reli kutoka Bandari ya Tanga hadi Kampala nchini Uganda.
“Kimsingi Jumuiya haina tatizo lolote kama watu wengi wanavyoaminishwa na vyombo vya habari, kilichopo ni tofauti ndogo za kimtazamo ambazo hazina madhara kwa ushawi wa Jumuiya,” alieleza msemaji huyo.
Jumuiya ya Afrika Mashariki ilianzishwa rasmi tena mwaka 1999 ikiwa na nchi wanachama waanzilishi ambazo ni Tanzania, Kenya na Uganda na baadaye kuongezeka Rwanda na Burundi, mwaka 2007
- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/makao-makuu-eac-kwafukuta#sthash.AwkNVAWF.dpuf

Share
Posted by Unknown
About the Author

Write admin description here..

0 comments:

Text Widget

Blogger templates. Proudly Powered by Blogger.