Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametangaza kuwa serikali yake
itapunguza kodi katika mishahara ya wafanyakazi kutoka asilimia 11 hadi kufikia
asilimia 9 kuanzia mwaka ujao wa fedha wa 2016/2017 ili kupunguza mzigo kwa
wafanyakazi.
Rais Magufuli
ametangaza uamuzi huo leo tarehe 01 Mei, 2016 wakati akihutubia katika sherehe
za maadhimisho ya siku ya siku ya wafanyakazi duniani, zilizofanyika kitaifa
katika uwanja wa Jamhuri Mjini Dodoma.
"Napenda kuwataarifa
kuwa serikali yangu kama nilivyoahidi wakati wa kampeni zangu, nimeamua
kupunguza kodi ya mapato ya mishahara kutoka asilimia 11 ya sasa hadi asilimia
9, kuanzia mwaka wa fedha wa 2016/2017, nikiwa nina mategemeo makubwa
waheshimiwa wabunge watapitisha bajeti ya serikali niliyoiwasilisha"
Amesema Dkt. Magufuli huku akishangiliwa na maelfu ya wafanyakazi waliojitokeza
uwanjani hapo.
Pamoja na uamuzi
huo, Rais Magufuli pia amewaahidi wafanyakazi kuwa baada ya kupunguza kodi
katika mishahara ya wafanyakazi, serikali yake itafanyia kazi mapendekezo ya
kuongeza mishahara.
Katika maadhimisho
hayo ambayo pia yamehudhuriwa na Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan,
Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa na Naibu Spika Dkt. Tulia Akson, Rais
Magufuli amewataka wafanyakazi kote nchini kushiriki kufanikisha Dira ya
Maendeleo ya Taifa ya 2025 kwa kufanya kazi kwa bidii, kujituma, weledi na
uadilifu.
Amesema Mpango wa
Maendeleo ya Taifa utagharimu takribani shilingi Trilioni 107 zikiwemo shilingi
Trilioni 59 kutoka serikalini, hivyo amewataka wafanyakazi wote kutambua kuwa
wanategemewa kuwaongoza watanzania kufanikisha upatikanaji wa fedha hizo kwa
kuchapa kazi.
Aidha, Rais
Magufuli amewataka wafanyakazi kuunga mkono juhudi za kuwafichua wanaozalisha
wafanyakazi hewa, huku akibainisha kuwa mpaka kufikia jana tarehe 30 Aprili,
2016 jumla ya wafanyakazi hewa waliobainika walikuwa 10,293 ambao kwa mwezi mmoja
tu wamelipwa shilingi bilioni 11.6.
"Kwa hiyo kwa
mwaka wafanyakazi hewa hawa wamekuwa wakilipwa shilingi 139,239,285,592.92,
ukizidisha kwa miaka mitano kama tungekuwa na wafanyakazi hewa, miaka mitano
tu, tusiseme miaka kumi au ishirini au kumi na ngapi, miaka mitano tu, manaake
wangelipwa shilingi 696,196,427,964.6.
"Hizi bilioni
696 zinatosha kujenga madaraja kama la Nyerere lililopo Kigamboni, madaraja
matatu, hizi bilioni 696 zinatosha kujenga flyover zinazojengwa Dar es salaam
kwa msaada na mkopo kutoka Japan, zingekuwa saba, hizi bilioni 696 mjiulize
kama zingetumika kulipa mishahara ya wafanyakazi waliopo ndani ya serikali,
tungewaongezea mshahara kiasi gani" amesisitiza
Rais Magufuli.
Hata hivyo Rais
Magufuli amewahakikishia wafanyakazi wote ambao wanatekeleza majukumu yao
kihalali kuwa serikali yake itawalinda na kuwatetea huku akitaka wawapuuze
wanaodai serikali ya awamu ya tano haiwapendi wafanyakazi.
"Tukumbuke ya
kuwa kazi ni utu, kazi sio fursa ya kupata mshahara kwa manufaa ya familia zetu
bali ni fursa nzuri ya kutoa mchango kwa taifa lako kwa manufaa ya kizazi cha
sasa na kijacho" amesema Dkt. Magufuli.
Gerson
Msigwa
Kaimu
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dodoma
01 Mei,
2016
0 comments: